Tuukomboe Wakati

 

Waefeso 5:16-17. “mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu”. “Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana”

Shalom. Leo tutafakari mambo machache tunapojiandaa kupokea mwaka 2017. 1. Tusiupokee mwaka kwa mazoea bali tujitafakari. Ukweli ni kwamba dunia inaingia 2017 lakini kifikra sio kila nchi au mtu amefika 2017. Kuna wengine muda wao umetekwa na hivyo hata 2016 kifikra bado hawajafika lakini wataupokea mwaka 2017 kimazoea tu na hawataona tofauti ktk maisha yao. Tunapaswa kuukomboa muda ambao adui ameuteka tukajikuta hatujafanya yale yaliyopasa.

Mfano mtu mlevi au mzinzi hawezi kufanya mambo na maamuzi sahihi maana anaishi muda tofauti na hali halisi. Unaweza kumkuta mtu ana miaka zaidi ya 40 lakini bado hajaoa anaendekeza zinaa tu. Maana yake muda wake ktk eneo la ndoa umetekwa. Mtu kama huyo anahitaji maombi ya kumfungua ili aweze kuukomboa huo muda. Ndio maana tunaona pia maendeleo ni tofauti baina ya mtu na mtu. Yule mtu anayeishi kwa nyakati halisi kifikra anakuwa na maendeleo kuliko yule ambaye fikra zake zimetekwa. Mtu unakuta ana miaka 50 lakini ana fikra za kijana wa miaka 30 hawezi kuwa na maendeleo.

2. Mungu ndiye kaweka majira na nyakati. MDO 17: 26-27. Lengo ni ili tumtafute na kufanya mapenzi yake. Fanya maamuzi kwamba mwaka 2017 utafanya mapenzi ya Mungu. Tutaweza kufanya mapenzi ya Mungu iwapo tutalubali kufanywa upya nia zetu. Biblia inasema: “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”. Warumi 12: 2 3. Tutambue hizi ni nyakati gani na tufanye yafaayo. Biblia inasema katika kila jambo kuna majira yake Mhubiri 3:1. Jambo linakuwa na faida tu likifanywa kwa wakati wake. Mfano msichana akiolewa akapata mtoto inakuwa ni shangwe na vigelegele. Lakini binti huyohuyo akizaa nyumbani bila kuolewa ni masononeko makubwa kwa wazazi.

Tudhamirie kwamba Mwaka 2017 tutafanya mambo kwa muda na majira yake. Mungu wetu ni Mungu anayefanya kazi zake kwa nyakati na majira hivyo tuji connect na Mungu ili tujue kile cha kufanya kila wakati. Tuwe kama wana wa Isakari maana ndipo tutakuwa juu. Biblia inasema: “Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao”. 1 Nyakati 12:32. Muwe na siku njema.

Comments

Popular posts from this blog

Aliyeko Juu Mngoje Chini!

Ukishindwa, Ongeza Uwezo!

Hope